Ufunuo wa Yohana - Sura ya 5

1Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba.
2Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, N'nani astahiliye kukifungua kitabu, na kuzivunja muhuri zake?
3Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama.
4Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama.
5Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.
6Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote.
7Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi.
8Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu.
9Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,
10ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.
11Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu,
12wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.
13Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele.
14Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.