Ufunuo wa Yohana - Sura ya 9

Ufunuo wa Yohana - Sura ya 9

1Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu.

2Akalifungua shimo la kuzimu; moshi ukapanda kutoka mle shimoni kama moshi wa tanuru kubwa; jua na anga vikatiwa giza kwa sababu ya ule moshi wa shimoni.

3Nzige wakatoka katika ule moshi, wakaenda juu ya nchi, wakapewa nguvu kama nguvu waliyo nayo nge wa nchi.

4Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu cho chote kilicho kibichi, wala mti wo wote, ila wale watu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao.

5Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe miezi mitano. Na maumivu yao yalikuwa kama kuumwa na nge, aumapo mwanadamu.

6Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia.

7Na maumbo ya hao nzige yalikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita, na juu ya vichwa vyao kama taji, mfano wa dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama nyuso za wanadamu.

8Nao walikuwa na nywele kama nywele za wanawake. Na meno yao yalikuwa kama meno ya simba.

9Nao walikuwa na dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani.

10Nao wana mikia kama ya nge, na miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia yao.

11Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni.

12Ole wa kwanza umekwisha pita. Tazama, bado ziko ole mbili, zinakuja baadaye.

13Malaika wa sita akapiga baragumu, nikasikia sauti moja iliyotoka katika zile pembe za madhabahu ya dhahabu iliyo mbele za Mungu,

14ikimwambia yule malaika wa sita aliyekuwa na baragumu, Wafungue nao malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Frati.

15Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu.

16Na hesabu ya majeshi ya wapanda farasi ilikuwa elfu ishirini mara elfu kumi; nilisikia hesabu yao.

17Hiyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao waliokaa juu yao, wana dirii kifuani, kama za moto, na za samawi, na za kiberiti; na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoka moto na moshi na kiberiti.

18Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kiberiti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao.

19Kwa maana nguvu za hao farasi ni katika vinywa vyao, na katika mikia yao; maana mikia yao ni mfano wa nyoka, ina vichwa, nao wanadhuru kwa hivyo.

20Na wanadamu waliosalia, wasiouawa kwa mapigo hayo, hawakuzitubia zile kazi za mikono yao, hata wasiwasujudie mashetani, na sanamu za dhahabu na za fedha na za shaba na za mawe na za miti, zisizoweza kuona wala kusikia wala kuenenda.

21Wala hawakuutubia uuaji wao, wala uchawi wao, wala uasherati wao, wala wivi wao.