Warumi - Sura ya 10

Warumi - Sura ya 10

1Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.

2Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa.

3Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.

4Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki.

5Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo.

6Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini),

7au, Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.)

8Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.

9Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.

10Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.

11Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.

12Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;

13kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.

14Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?

15Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!

16Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu?

17Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.

18Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.

19Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena,

20Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema,

21Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa naliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.