Warumi - Sura ya 16

Warumi - Sura ya 16

1Namkabidhi kwenu Fibi, ndugu yetu, aliye mhudumu wa kanisa lililoko Kenkrea;

2kwamba mmpokee katika Bwana, kama iwapasavyo watakatifu; mkamsaidie katika neno lo lote atakalohitaji kwenu; kwa sababu yeye naye amekuwa msaidizi wa watu wengi, akanisaidia mimi pia.

3Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu;

4waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu; ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao.

5Nisalimieni Epaineto, mpenzi wangu, aliye malimbuko ya Asia kwa Kristo.

6Nisalimieni Mariamu, aliyejitaabisha sana kwa ajili yenu.

7Nisalimieni Androniko na Yunia, jamaa zangu, waliofungwa pamoja nami, ambao ni maarufu miongoni mwa mitume; nao walikuwa katika Kristo kabla yangu.

8Nisalimieni Ampliato, mpenzi wangu katika Bwana.

9Nisalimieni Urbano, mtenda kazi pamoja nami katika Kristo, na Stakisi, mpenzi wangu.

10Nisalimieni Apele, mwenye kukubaliwa katika Kristo. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Aristobulo.

11Nisalimieni Herodioni, jamaa yangu. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Narkiso, walio katika Bwana.

12Nisalimieni Trifaina na Trifosa, wenye bidii katika Bwana. Nisalimieni Persisi, mpenzi aliyejitahidi sana katika Bwana.

13Nisalimieni Rufo, mteule katika Bwana, na mamaye, aliye mama yangu pia.

14Nisalimieni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma, na ndugu walio pamoja nao.

15Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa, na watakatifu wote walio pamoja nao.

16Salimianeni kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo yawasalimu.

17Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao.

18Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu.

19Maana utii wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya.

20Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. [Amina.]

21Timotheo, mtenda kazi pamoja nami, awasalimu, na Lukio, na Yasoni, na Sosipatro, jamaa zangu.

22Mimi Tertio, niliyeandika waraka huu, nawasalimu katika Bwana.

23Gayo, mwenyeji wangu na wa Kanisa lote pia awasalimu. Erasto, wakili wa mji, awasalimu, na Kwarto, ndugu yetu.

24Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.]

25Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele,

26ikadhihirishwa wakati huu kwa maandiko ya manabii, ikajulikana na mataifa yote kama alivyoamuru Mungu wa milele, ili waitii Imani.

27Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele. Amina.