Warumi - Sura ya 3

Warumi - Sura ya 3

1Basi Myahudi ana ziada gani? Na kutahiriwa kwafaa nini?

2Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu.

3Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! Kutokuamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu?

4Hasha! Mungu aonekane kuwa amini na kila mtu mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulike kuwa una haki katika maneno yako, Ukashinde uingiapo katika hukumu.

5Lakini, ikiwa udhalimu wetu waithibitisha haki ya Mungu, tuseme nini? Je! Mungu ni dhalimu aletaye ghadhabu? (Nasema kwa jinsi ya kibinadamu.)

6Hasha! Kwa maana hapo Mungu atawezaje kuuhukumu ulimwengu?

7Lakini, ikiwa kweli ya Mungu imezidi kudhihirisha utukufu wake kwa sababu ya uongo wangu, mbona mimi ningali nahukumiwa kuwa ni mwenye dhambi?

8Kwa nini tusiseme (kama tulivyosingiziwa, na kama wengine wanavyokaza kusema ya kwamba twasema hivyo), Na tufanye mabaya, ili yaje mema? Ambao kuhukumiwa kwao kuna haki.

9Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi;

10kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja.

11Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu.

12Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.

13Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao.

14Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.

15Miguu yao ina mbio kumwaga damu.

16Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao.

17Wala njia ya amani hawakuijua.

18Kumcha Mungu hakupo machoni pao.

19Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu;

20kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.

21Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii;

22ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;

23kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;

24wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;

25ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho

26apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.

27Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani.

28Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.

29Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia;

30kama kwa kweli Mungu ni mmoja, atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika imani, nao wale wasiotahiriwa atawahesabia haki kwa njia ya imani iyo hiyo.

31Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.