Warumi - Sura ya 6

Warumi - Sura ya 6

1Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi?

2Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?

3Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?

4Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

5Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake;

6mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;

7kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.

8Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye;

9tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena.

10Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu.

11Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.

12Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake;

13wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki.

14Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema.

15Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha!

16Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.

17Lakini Mungu na ashukuriwe, kwa maana mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake;

18na mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mkawa watumwa wa haki.

19Nasema kwa jinsi ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu. Kwa kuwa kama mlivyovitoa viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa.

20Kwa maana mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na haki.

21Ni faida gani basi mliyopata siku zile kwa mambo hayo mnayoyatahayarikia sasa? Kwa maana mwisho wa mambo hayo ni mauti.

22Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.

23Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.