Ruthi - Sura ya 2

Ruthi - Sura ya 2

1Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi.

2Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda.

3Basi akaenda, akaja akaokota masazo kondeni nyuma ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki.

4Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu kawaamkia wavunaji, akasema, Bwana akae nanyi. Nao wakamwitikia, Bwana na akubariki.

5Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani?

6Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu;

7naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota masazo, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hata sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo.

8Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu.

9Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana.

10Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni?

11Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo.

12Bwana akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake.

13Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako.

14Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza.

15Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee.

16Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze.

17Basi Ruthu akaokota masazo kondeni hata jioni; kisha akazipura zile nafaka alizoziokota, zikawa yapata efa moja ya shayiri.

18Akajitwika, akaenda zake mjini. Akamwonyesha mkwewe zile alizoziokota; akavitoa vile vyakula alivyovisaza alipokwisha kushiba, akampa.

19Basi mkwewe akamwuliza, Je! Umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Na abarikiwe yeye aliyekufahamu. Naye akamwarifu mkwewe ni nani ambaye alifanya kazi kwake, akasema, Yule mtu niliyefanya kazi kwake leo jina lake aitwa Boazi.

20Naye Naomi akamwambia mkwewe, Na abarikiwe huyo na Bwana, ambaye hakuuacha wema wake, wala kwa hao walio hai wala kwao waliokufa. Kisha Naomi akamwambia, Mtu huyu ni wa mbari yetu, mmojawapo wa jamaa yetu aliye karibu.

21Naye Ruthu Mmoabi akasema, Naam, akaniambia, Ukae papa hapa karibu na vijana wangu, hata watakapomaliza mavuno yangu yote.

22Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, Mwanangu, ni vizuri wewe ufuatane na wasichana wake, wala watu wasikukute katika konde linginelo lote.

23Hivyo yeye akafuatana na wasichana wake Boazi na kuokota, hata mwisho wa mavuno ya shayiri na mavuno ya ngano pia; naye alikuwa akikaa kwa mkwewe.