Ruthi - Sura ya 3

Ruthi - Sura ya 3

1Kisha Naomi akamwambia mkwewe, Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema?

2Basi na huyu Boazi, je! Siye wa mbari yetu, ambaye ulikuwapo pamoja na wasichana wake? Tazama, usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani.

3Basi wewe oga, ujipake mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa.

4Nayo itakuwa wakati atakapolala, utapaangalia mahali alalapo, nawe uingie, uifunue miguu yake ujilaze hapo; na yeye atakuambia utakalofanya.

5Akamwambia, Hayo yote unenayo mimi nitayafanya.

6Basi akashuka mpaka ugani; akafanya yote kama vile mkwewe alivyomwagiza.

7Ikawa huyo Boazi alipokwisha kula na kunywa, na moyo wake umekunjuka, alikwenda kulala penye mwisho wa chungu ya nafaka; na huyo mwanamke akaja taratibu, akaifunua miguu yake, akajilaza papo hapo.

8Na ikawa usiku wa manane yule mtu akasituka, akajigeuza; na kumbe! Yupo mwanamke amelala miguuni pake.

9Akasema, Ama! Ni nani wewe? Akamjibu, Ni mimi, Ruthu, mjakazi wako; uitande nguo yako juu ya mjakazi wako; kwa kuwa ndiwe wa jamaa aliye karibu.

10Akamwambia, Mwanangu, ubarikiwe na Bwana; umezidi kuonyesha fadhili zako mwisho kuliko mwanzo, kwa vile usivyowafuata vijana, kama ni maskini kama ni matajiri.

11Basi, mwanangu, usiogope; mimi nitakufanyia yote uyanenayo; kwa maana mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema.

12Tena ndiyo kweli ya kuwa mimi ni wa jamaa yako aliye karibu; lakini kuna mtu wa jamaa aliye karibu kuliko mimi.

13Wewe ungoje usiku huu; kisha, asubuhi, kama akikubali kukufanyia impasavyo jamaa, haya, na akufanyie; lakini ikiwa hataki yeye, basi mimi nitakufanyia impasavyo jamaa; Bwana aishivyo. Ulale wewe hata asubuhi.

14Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hata asubuhi; akaondoka mapema asijaweza mtu kumtambua mwenziwe; maana Boazi amesema, Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika penye uga.

15Tena alisema, Lete hapa shela yako uliyoivaa, uishike; naye akaishika; naye akampimia vipimo sita vya shayiri akamtwika; kisha huyo mwanamke akaenda zake mjini.

16Basi alipofika kwa mkwewe, huyo akamwuliza, Je! Mwanangu, imekuwaje? Akamwambia yote yule mtu aliyomfanyia.

17Akasema, Na vipimo hivi sita vya shayiri amenipa; maana akaniambia, Usiende kwa mkweo mikono mitupu.

18Naye mkwewe akasema, Basi, mwanangu, tulia; hata utakapojua jinsi litakavyotukia jambo hili; kwa sababu mtu huyu hataridhika, asipolimaliza jambo hilo leo.