Ruthi - Sura ya 4

Ruthi - Sura ya 4

1Basi Boazi akakwea kwenda mpaka langoni, akaketi pale; na tazama, yule mtu wa jamaa aliyekuwa karibu, ambaye Boazi amemnena, akapita. Naye akamwita, Haya! Wewe, karibu, uketi hapa. Naye akaja akaketi.

2Kisha akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, Ninyi nanyi, ketini hapa. Wakaketi.

3Kisha akamwambia yule jamaa, Huyu Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi aliyokuwa nayo ndugu yetu, Elimeleki;

4nami ilikuwa nia yangu nikujulishe wewe, na kukuambia, Uinunue mbele ya hawa waliopo na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya, uikomboe; lakini kama hutaikomboa, uniambie ili nijue mimi; kwa kuwa hakuna mtu wa kuikomboa ila wewe, na baada yako ni mimi. Naye akasema, Nitaikomboa mimi.

5Ndipo Boazi aliposema, Siku ile utakapolinunua shamba mkononi mwa Naomi, unamnunua Ruthu pia, huyu Mmoabi, mkewe marehemu, ili makusudi umwinulie marehemu jina katika urithi wake.

6Basi yule jamaa aliyekuwa wa karibu akasema, Mimi sitaweza kulikomboa kwa nafsi yangu, nisije nikauharibu urithi wangu mwenyewe; basi haki yangu ya kulikomboa ujichukulie wewe, maana mimi sitaweza kulikomboa.

7Basi hii ilikuwa desturi zamani za kale katika Israeli, kwa habari ya kukomboa na kubadiliana, ili kuyahakikisha yote; mtu huvua kiatu chake na kumpa mwenziwe; ndivyo walivyohakikisha neno katika Israeli.

8Basi yule jamaa akamwambia Boazi, Wewe ujinunulie mwenyewe. Akavua kiatu chake.

9Naye Boazi akawaambia wale wazee na watu wote, Leo hivi ninyi ni mashahidi ya kwamba mimi nimenunua yote yaliyokuwa ya Elimeleki, na yote yaliyokuwa ya Kilioni na Maloni, mkononi mwa Naomi.

10Tena, huyu Ruthu Mmoabi, mkewe Maloni, nimemnunua awe mke wangu, makusudi nipate kumwinulia marehemu jina katika urithi wake, jina lake marehemu lisikatike miongoni mwa ndugu zake, wala langoni pa mji wake; leo hivi ninyi ni mashahidi.

11Na watu wote waliokuwapo langoni, na wale wazee, wakasema, Naam, sisi ni mashahidi. Bwana na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wawili walioijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata, na kuwa mashuhuri katika Bethlehemu.

12Nyumba yako na ifanane na nyumba yake Peresi, ambaye kwamba Tamari alimzalia Yuda, kwa wazao atakaokupa Bwana katika mwanamke huyu.

13Basi Boazi akamtwaa Ruthu, naye akawa mke wake; naye akaingia kwake, na Bwana akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa mtoto wa kiume.

14Nao wale wanawake wakamwambia Naomi, Na ahimidiwe Bwana, asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli.

15Naye atakurejezea uhai wako, na kukuangalia katika uzee wako; kwa maana mkweo, ambaye akupenda, naye anakufaa kuliko watoto saba, ndiye aliyemzaa.

16Basi Naomi akamtwaa yule mtoto, akamweka kifuani pake, akawa mlezi wake.

17Nao wale wanawake waliokuwa jirani zake wakampa jina, wakisema, Naomi amezaliwa mwana; wakamwita jina lake Obedi; yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi.

18Hivi ndivyo vizazi vya Peresi; Peresi alimzaa Hesroni;

19na Hesroni akamzaa Ramu; na Ramu akamzaa Aminadabu;

20na Aminadabu akamzaa Nashoni; na Nashoni akamzaa Salmoni;

21na Salmoni akamzaa Boazi; na Boazi akamzaa Obedi;

22na Obedi akamzaa Yese; na Yese akamzaa Daudi.