Wimbo Ulio Bora - Sura ya 1

Wimbo Ulio Bora - Sura ya 1

1Wimbo ulio bora, wa Sulemani.

2Kubusu na anibusu kwa kinywa chake. Maana pambaja zako zapita divai;

3Manukato yako yanukia vizuri; Jina lako ni kama marhamu iliyomiminwa; Kwa hiyo wanawali hukupenda.

4Nivute nyuma yako, na tukimbie; Mfalme ameniingiza vyumbani mwake. Tutafurahi na kukushangilia; Tutazinena pambaja zako kuliko divai; Ndiyo, ina haki wakupende.

5Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri, Enyi binti za Yerusalemu, Mfano wa hema za Kedari, Kama mapazia yake Sulemani.

6Msinichunguze kwa kuwa ni mweusi-mweusi, Kwa sababu jua limeniunguza. Wana wa mamangu walinikasirikia, Waliniweka niwe mlinzi wa mashamba ya mizabibu; Bali shamba langu mwenyewe sikulilinda.

7Nijulishe, ee mpendwa wa nafsi yangu, Ni wapi utakapolisha kundi lako, Ni wapi utakapolilaza adhuhuri. Kwa nini niwe kama aliyefungiwa kidoto, Karibu na makundi ya wenzako?

8Usipojua, wewe uliye mzuri katika wanawake, Shika njia uzifuate nyayo za kondoo, Na kuwalisha wana-mbuzi wako Karibu na hema za wachungaji.

9Mpenzi wangu, nimekulinganisha Na farasi katika magari ya Farao.

10Mashavu yako ni mazuri kwa mashada, Shingo yako kwa mikufu ya vito.

11Tutakufanyizia mashada ya dhahabu, Yenye vifungo vya fedha.

12Muda mfalme alipoketi juu ya matakia, Nardo yangu ilitoa harufu yake.

13Mpendwa wangu ni kama mfuko wa manemane Ukilazwa usiku maziwani mwangu.

14Mpendwa wangu ni kama kishada cha hina, Katika mizabibu huko Engedi.

15Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua.

16Tazama, u mzuri, mpendwa wangu, Wapendeza, na kitanda chetu ni majani;

17Nguzo za nyumba yetu ni mierezi, Na viguzo vyetu ni miberoshi.