Wimbo Ulio Bora - Sura ya 2

Wimbo Ulio Bora - Sura ya 2

1Mimi ni ua la uwandani,

2Kama nyinyoro kati ya miiba, Kadhalika mpenzi wangu kati ya binti.

3Kama mpera kati ya miti ya msituni, Kadhalika mpendwa wangu kati ya vijana. Naliketi kivulini mwake kwa furaha, Na matunda yake naliyaonja kuwa matamu.

4Akanileta mpaka nyumba ya karamu, Na bendera yake juu yangu ni mapenzi.

5Nishibisheni zabibu, niburudisheni kwa mapera, Kwa maana nimezimia kwa mapenzi.

6Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, Nao wa kuume unanikumbatia!

7Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.

8Sikiliza! Ni mpendwa wangu! Tazama, anakuja, Akiruka milimani, akichachawa vilimani.

9Mpendwa wangu ni kama paa, au ayala. Tazama, asimama nyuma ya ukuta wetu, Achungulia dirishani, atazama kimiani.

10Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,

11Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda zake;

12Maua yatokea katika nchi, Wakati wa kupelea umefika, Na sauti ya mwigo husikiwa kwetu.

13Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako.

14Hua wangu, mafichoni mwa jabali, Katika sitara za magenge, Nitazame uso wako, nisikie sauti yako, Maana sauti yako ni tamu na uso wako mzuri.

15Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.

16Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake; Hulisha kundi lake penye nyinyoro.

17Hata jua lipunge, na vivuli vikimbie, Unigeukie, mpendwa wangu, Nawe uwe kama paa, au ayala, Juu ya milima ya Betheri.