Wimbo Ulio Bora - Sura ya 4

Wimbo Ulio Bora - Sura ya 4

1Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua, Nyuma ya barakoa yako. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi, Wakijilaza mbavuni pa mlima Gileadi.

2Meno yako ni kama kundi waliokatwa manyoya, Wakipanda kutoka kuoshwa, Ambao kila mmoja amezaa mapacha, Wala hakuna aliyefiwa kati yao.

3Midomo yako ni kama uzi mwekundu, Na kinywa chako ni kizuri; Mashavu yako ni kama kipande cha komamanga, Nyuma ya barakoa yako.

4Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, Uliojengwa pa kuwekea silaha; Ngao elfu zimetungikwa juu yake, Zote ni ngao za mashujaa.

5Maziwa yako mawili ni kama wana-paa wawili, Nyuma ya barakoa yako. Ambao ni mapacha ya paa; Wakilisha penye nyinyoro.

6Hata jua lipunge, na vivuli vikimbie, Nitakwenda kwenye mlima wa manemane, Na kwenye kilima cha ubani.

7Mpenzi wangu, u mzuri pia pia, Wala ndani yako hamna ila.

8Bibi arusi, njoo pamoja nami toka Lebanoni, Pamoja nami toka Lebanoni. Shuka kutoka kilele cha Amana, Kutoka vilele vya Seniri na Hermoni; Kutoka mapangoni mwa simba, Kutoka milimani mwa chui.

9Umenishangaza moyo, umbu langu, Bibi arusi, umenishangaza moyo, Kwa mtupo mmoja wa macho yako, Kwa mkufu mmoja wa shingo yako.

10Jinsi zilivyo nzuri pambaja zako, umbu langu, Bibi arusi, ni nzuri kupita divai; Na harufu ya marhamu yako Yapita manukato ya kila namna.

11Bibi arusi, midomo yako yadondoza asali, Asali na maziwa vi chini ya ulimi wako; Na harufu ya mavazi yako Ni kama harufu ya Lebanoni.

12Bustani iliyofungwa ni umbu langu, bibi arusi, Kijito kilichofungwa, chemchemi iliyotiwa muhuri.

13Machipuko yako ni bustani ya komamanga, Yenye matunda mazuri, hina na nardo,

14Nardo na zafarani, mchai na mdalasini, Na miti yote iletayo ubani, Manemane na udi, na kolezi kuu zote.

15Wewe ndiwe chemchemi ya bustani yangu, Kisima cha maji yaliyo hai, Vijito vya Lebanoni viendavyo kasi.

16Amka, kaskazi; nawe uje, kusi; Vumeni juu ya bustani yangu, Manukato ya bustani yatokee. Mpendwa wangu na aingie bustanini mwake, Akayale matunda yake mazuri.