Wimbo Ulio Bora - Sura ya 5

Wimbo Ulio Bora - Sura ya 5

1Naingia bustanini mwangu, umbu langu, bibi arusi, Nachuma manemane yangu na rihani, Nala sega la asali na asali yangu, Nanywa divai yangu na maziwa. Kaleni, rafiki zangu, kanyweni, Naam, nyweni sana, wapendwa wangu.

2Nalikuwa nimelala, lakini moyo wangu u macho, Sikiliza! Mpendwa wangu anabisha! Nifungulie, umbu langu, mpenzi wangu, Hua wangu, mkamilifu wangu, Kwa maana kichwa changu kimelowa umande, Nywele zangu zina manyunyu ya usiku.

3Nimeivua kanzu yangu; niivaeje? Nimeitawadha miguu; niichafueje?

4Mpendwa wangu aliutia mkono wake tunduni, Na moyo wangu ukachomeka kwa ajili yake.

5Nikaondoka nimfungulie mpendwa wangu; Mikono yangu ilidondoza manemane, Na vidole vyangu matone ya manemane, Penye vipini vya komeo.

6Nalimfungulia mpendwa wangu, Lakini mpendwa wangu amegeuka amepita; (Nimezimia nafsi yangu aliponena), Nikamtafuta, nisimpate, Nikamwita, asiniitikie.

7Walinzi wazungukao mjini waliniona, Wakanipiga na kunitia jeraha, Walinzi walindao kuta zake Wakaninyang'anya shela yangu.

8Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Ninyi mkimwona mpendwa wangu, Ni nini mtakayomwambia? Ya kwamba nazimia kwa mapenzi.

9Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako, Wewe uliye mzuri katika wanawake, Mpendwa wa namna gani ni mpendwa wako, Hata wewe utusihi hivyo?

10Mpendwa wangu ni mweupe, tena mwekundu, Mashuhuri miongoni mwa elfu kumi;

11Kichwa chake ni kama dhahabu safi sana, Nywele zake ni za ukoka, nyeusi kama kunguru;

12Macho yake ni kama hua penye vijito, Wakioga kwa maziwa, wakiikalia mito iliyojaa;

13Mashavu yake ni kama matuta ya rihani, Ambayo hufanyizwa manukato; Midomo yake ni kama nyinyoro, Inadondoza matone ya manemane;

14Mikono yake ni kama mianzi ya dhahabu, lliyopambwa kwa zabarajadi; Kiwiliwili chake kama kazi ya pembe, Iliyonakishiwa kwa yakuti samawi;

15Miguu yake ni kama nguzo za marimari, Zilizowekwa juu ya misingi ya dhahabu; Sura yake ni kama Lebanoni, Ni bora mfano wa mierezi;

16Kinywa chake kimejaa maneno matamu, Ndiye mzuri sana pia pia. Ni huyu mpendwa wangu, ni huyu rafiki yangu, Enyi binti za Yerusalemu.