Tito - Sura ya 2

1Lakini wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima;
2ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi.
3Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema;
4ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;
5na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.
6Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi;
7katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu,
8na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu.
9Watumwa na wawatii bwana zao, wakiwapendeza katika mambo yote; wasiwe wenye kujibu,
10wasiwe waibaji; bali wauonyeshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote.
11Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;
12nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;
13tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;
14ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.
15Nena maneno hayo, onya na kukaripia kwa mamlaka yote; asikudharau mtu awaye yote.