Tito - Sura ya 3

1Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema;
2wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote.
3Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana.
4Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa;
5si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu;
6ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu;
7ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.
8Ni neno la kuaminiwa; na mambo hayo nataka uyanene kwa nguvu, ili wale waliomwamini Mungu wakumbuke kudumu katika matendo mema. Hayo ni mazuri, tena yana faida kwa wanadamu.
9Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana.
10Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae;
11ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe.
12Wakati nitakapomtuma Artema kwako au Tikiko, jitahidi kuja kwangu huku Nikopoli; kwa maana huku nimekusudia kukaa wakati wa baridi.
13Zena, yule mwana-sheria, na Apolo, uwasafirishe kwa bidii, wasipungukiwe na cho chote.
14Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema, kwa matumizi yaliyo lazima, ili wasiwe hawana matunda.
15Watu wote walio pamoja nami wakusalimu. Tusalimie wale watupendao katika imani. Neema na iwe pamoja nanyi nyote.