Zekaria - Sura ya 12

Zekaria - Sura ya 12

1Ufunuo wa neno la Bwana juu ya Israeli. Haya ndiyo asemayo Bwana, azitandaye mbingu, auwekaye msingi wa dunia, aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake.

2Angalia, mimi nitafanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumba-yumba kwa watu wa kabila zote, wazungukao pande zote; tena kitakuwa juu ya Yuda pia wakati wa kuhusuriwa Yerusalemu.

3Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake.

4Katika siku hiyo, asema Bwana, nitamtia kila farasi ushangao, na yeye ampandaye nitamtia wazimu; nami nitaifunulia nyumba ya Yuda macho yangu, nami nitamtia upofu kila farasi wa hizo kabila za watu.

5Na wakuu wa Yuda watasema mioyoni mwao, Wenyeji wa Yerusalemu ni nguvu zangu katika Bwana wa majeshi, Mungu wao.

6Siku hiyo nitawafanya wakuu wa Yuda kuwa kama kigae chenye moto katika kuni, na kama kinga cha moto katika miganda; nao watateketeza watu wa kila kabila, wawazungukao pande zote, upande wa mkono wa kuume na upande wa mkono wa kushoto; na baada ya haya Yerusalemu utakaa mahali pake, naam, hapo Yerusalemu.

7Naye Bwana ataziokoa hema za Yuda kwanza, ili utukufu wa nyumba ya Daudi, na utukufu wa wenyeji wa Yerusalemu, usipate kutukuzwa kuliko Yuda.

8Katika siku hiyo Bwana atawalinda wenyeji wa Yerusalemu; na yeye aliye dhaifu miongoni mwao atakuwa kama Daudi siku hiyo; nayo nyumba ya Daudi itakuwa kama Mungu, kama malaika wa Bwana mbele yao.

9Hata itakuwa siku hiyo, ya kwamba nitatafuta kuwaangamiza mataifa yote watakaokuja kupigana na Yerusalemu.

10Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.

11Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.

12Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;

13jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.

14Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao.