Zekaria - Sura ya 2

1Kisha nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake.
2Ndipo nikasema, Unakwenda wapi? Akaniambia, Ninakwenda kuupima Yerusalemu, nione upana wake ulivyo na urefu wake ulivyo.
3Na tazama, yule malaika aliyesema nami akasimama karibu, na malaika mwingine akatoka ili kuonana naye;
4naye akamwambia, Piga mbio, kamwambie kijana huyu, na kusema, Yerusalemu utakaliwa na watu, kama vijiji visivyo na kuta, kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo ndani yake.
5Kwa maana mimi, asema Bwana, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani yake.
6Haya! Haya! Ikimbieni nchi ya kaskazini, asema Bwana; kwa maana mimi nimewatawanya ninyi kama pepo nne za mbinguni, asema Bwana.
7Haya! Ee Sayuni, jiponye, wewe ukaaye pamoja na binti Babeli.
8Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.
9Kwa maana, tazama, nitatikisa mkono wangu juu yao, nao watakuwa mateka ya hao waliowatumikia; nanyi mtajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma.
10Imba, ufurahi, Ee binti Sayuni; maana, tazama, ninakuja, nami nitakaa kati yako, asema Bwana.
11Na mataifa mengi watajiunga na Bwana katika siku ile, nao watakuwa watu wangu; nami nitakaa kati yako, nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwako.
12Na Bwana atairithi Yuda, iwe sehemu yake katika nchi takatifu, naye atachagua Yerusalemu tena.
13Nyamazeni, ninyi nyote wenye mwili, mbele za Bwana; kwa maana ameamka, na kutoka katika maskani yake takatifu.