Zekaria - Sura ya 9
1Ufunuo wa neno la Bwana, lililosemwa juu ya nchi ya Hadraki, na Dameski itakuwa mahali pake pa kustarehe; kwa maana jicho la mwanadamu na la kabila zote za Israeli linamwelekea Bwana;
2na Hamathi pia iliyo mpakani mwake; na Tiro, na Sidoni, kwa maana ana akili nyingi.
3Na Tiro alijijengea ngome, akakusanya fedha kama mchanga, dhahabu safi kama matope ya njia kuu.
4Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto.
5Ashkeloni ataona haya na kuogopa; Gaza pia, naye atafadhaika sana; na Ekroni, kwa maana taraja lake litatahayarika; na mfalme ataangamia toka Gaza, na Ashkeloni atakuwa hana watu.
6Na mwana wa haramu atatawala huko Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.
7Nami nitaondoa damu yake kinywani mwake, na machukizo yake nitayatoa katika meno yake; yeye naye atakuwa ni mabaki kwa Mungu wetu; naye atakuwa kama mtu mkuu katika Yuda, na Ekroni kama Myebusi.
8Nami nitapiga kambi yangu pande zote za nyumba yangu ili kuwapinga adui, mtu awaye yote asipite ndani yake wala kurudi; wala mtu aoneaye hatapita tena kati yao; kwa maana sasa nimeona kwa macho yangu.
9Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.
10Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.
11Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji.
12Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu.
13Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawaondokesha wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Uyunani, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa.
14Naye Bwana ataonekana juu yao, Na mshale wake utatoka kama umeme; Na Bwana MUNGU ataipiga tarumbeta, Naye atakwenda kwa pepo za kisulisuli za kusini.
15Bwana wa majeshi atawalinda; Nao watakula na kuyakanyaga mawe ya teo; Nao watakunywa na kufanya kelele kama kwa divai; Nao watajazwa kama mabakuli, kama pembe za madhabahu.
16Na Bwana, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo, Kama kundi la watu wake; Kwa maana watakuwa kama vito vya taji, Vikimeta-meta juu ya nchi yake.
17Maana wema wake, jinsi ulivyo mwingi! Na uzuri wake, jinsi ulivyo mwingi! Nafaka itawasitawisha vijana wanaume, Na divai mpya vijana wanawake.

Swahili
Italiano (it-IT)
Português do Brasil (pt-BR)
Polski (PL)
Deutsch (Deutschland)
Français (France)
Español (España)
Українська Біблія у перекладі Огієнка
English Bible - 21ST CENTURY KING JAMES (KJ21)